

……………………………………………………
Na Mwandishi wetu
MTANDAO wa Radio za Kijamii nchini Tanzania (COMNETA) na Chuo Kikuu Huria (OUT) kwa umoja wao zimepongeza mchango mkubwa wa aliyekuwa Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Tolly Mbwete kwa jitihada zake za kuziunganisha redio jamii na chuo kuhakikisha taarifa zinawafikia walio wengi hasa vijijini.
Katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa OUT hivi karibuni mtandao wa COMNETA umesema jitihada za Profesa Mbwete kuziunganisha taasisi hizo mbili zimefanikishwa kwa kiasi kikubwa kufikisha taarifa za kozi mbalimbali zinazoendesha chuoni na kwa bei nafuu kwa Watanzania wengi ambao umesaidia kukifahamu na hatimae kujiunga na chuo.
Akisoma risala fupi iliyotayarishwa na COMNETA, Katibu wa mtandao huo Riziki Leisuya alisema kwamba makubaliano na mashirikiano kati ya Comneta na OUT yaliyowezeshwa na Profesa Mbwete yamezaa matunda mengi baina ya pande hizo mbili kiasi cha kulishawishi Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu ,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kukubali kujenga studio ya redio katika chuo hicho ili kurahisisha mawasiliano kwa kutayarisha vipindi lakini pia itatumika na wanafunzi wanaochukua taaluma ya uandishi kufanya mazoezi kwa vitendo kuboresha mafunzo yao.
“Comneta kupitia redio zake imefanikiwa kupeleka habari wilayani na vijijini kwa kukitangaza chuo kwa watu wasiojiweza jambo ambalo limesababisha ongezeko la idadi ya wanafunzi chuoni hapo kutokana na unafuu wa gharama” iliongeza risala hiyo iliyosomwa na Riziki.
Profesa Mbwete ambaye muda wake wa utumishi chuoni hapo umefikia kikomo kwa sasa amechaguliwa kuwa Mkuu wa Vyuo Vikuu vya Kikanda (Pan African Universities-PAU) na Umoja wa Nchi huru za Afrika kuanzia mwezi Januari mwaka 2015.
Akiwashukuru na kuwaaga wana-Comneta ambao walihudhuria ulingo wa siku tatu kutathminimradi wa demokrasia na Amani (DEP) Profesa Mbwete alisema amefarijika na ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo mbili ambao umekuwa na mafanikio ya kipekee kwa umma wa Tanzania na kuahidi kumkabidhi atakayechukua nafasi yake kuendeleza ushirikiano huo na kumshauri ofisi ya COMNETA iendelee kwa mkataba wa ushirikiano kwa miaka mitatu na kila mwaka kuufanyika mapitio na mrejesho.
Naye Balozi Christopher Liundi ambaye ni mshauri wa Unesco akimzungumzia Profesa Mbwete alisema kwamba Profesa Mbwete anastahili pongezi kutokana na jinsi alivyoimarisha Chuo Kikuu Huria na kuimarisha ushirikiano kati ya Chuo hicho na Comneta kwa kutoa ofisi ambayo mtandao wa redio za jamii unaitumia kwa kutekeleza majukumu yake kama jitihada za kutoa uwezo kwa mtandao huo.
“Profesa Mbwete alikuwa mstari wa mbele kupanua chuo na namshukuru sana kwa kauli yake ya kuipa COMNETA miaka mingine mitatu kutumia ofisi iliyotolewa na chuo chini ya usimamizi wake. Ninaamini kwamba huko aendako atapeperusha bendera ya Tanzania na ataiwakilisha vizuri kwenye PAU, nina matarajio makubwa sana kutoka kwake,’ alisema Balozi Christopher Liundi.



